Baraza la Taifa la Usimamizi wa Haki, NCAJ limepitisha mageuzi mbalimbali yanayolenga kuimarisha utoaji wa huduma za haki, kuboresha ushirikiano kati ya taasisi za sekta ya haki na kuongeza upatikanaji wa haki nchini.
Katika kikao cha 38 Baraza hilo lilithibitisha tena dhamira yake ya kujenga mfumo wa haki unaomweka mwananchi mbele, likikanusha madai ya kuwepo kwa mzozo katika sekta hiyo.
Wakiongozwa na Jaji Mkuu Martha Koome, wanachama wa NCAJ wanahakikishia Wakenya kuwa taasisi za haki zinaendelea kushirikiana kwa karibu na kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Miongoni mwa maazimio muhimu yaliyopitishwa ni kuidhinishwa kwa Rasimu ya Mswada wa Makosa ya Kujamiiana wa mwaka 2026, unaolenga kukabiliana na aina mpya za ukatili wa kijinsia na kingono, yakiwemo makosa yanayotekelezwa kwa kutumia teknolojia, huku ukiimarisha ulinzi wa kisheria kwa manusura.
Baraza lilifufua pia Kamati Maalum ya Maandalizi ya Uchaguzi, inayoongozwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC kuratibu maandalizi ya sekta ya haki kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.
Maazimio mengine yanajumuisha kuimarisha mapambano dhidi ya uhalifu wa wanyamapori, kuidhinisha Fomu mpya ya Utambuzi wa Washukiwa kwa matumizi ya Huduma ya Kitaifa ya Polisi, kuchunguza uwezekano wa kuanzisha Mahakama Maalum za Matibabu na Urekebishaji na Magereza Huria na kupitisha mwongozo wa kitaifa wa kuwahoji watoto ndani ya mfumo wa haki.
Baraza pia liliahidi kuharakisha matumizi ya teknolojia katika sekta ya haki, kupunguza mrundikano wa kesi mahakamani na kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za haki ili kuhakikisha Wakenya wote wanapata haki kwa wakati, kwa usawa na kwa uwajibikaji.