Jumla ya watu milioni 28 wameazima fedha kutoka kwa Hazina ya Hustler (Hustler Fund) hadi kufikia sasa.
Rais William Ruto amesema jumla ya shilingi bilioni 90, zinazotolewa kwa aina tatu, zimekopeshwa watu hao.
Fedha hizo zinatolewa kama Mkopo wa Kibinafsi, Mkopo wa Kuziba Pengo na Makundi ya Hasla.
Rais Ruto akiahidi kuwa serikali itafanya kila iwezalo kuhakikisha hazina hiyo, inayotoa mkopo wa shilingi milioni 50 kwa siku, una fedha za kutosha kukidhi mahitaji ya wanaouhitaji.
Akizungumza alipoarifiwa kuhusu utendaji wa hazina hiyo tangu kuzinduliwa kwake mwezi Novemba mwaka 2022, Rais alidokeza kuwa jumla ya wateja milioni 10 wamekopa fedha mara mbili huku wateja milioni 4.5 wakiwa na alama nzuri za A na B, ikiwa na maana kwamba wao hukopa na kisha kulipa madeni yao.
Kumekuwa na visa vilivyoripotiwa vya Wakenya kukopa fedha kwenye hazina hiyo na kisha kutowajibika kwa kulipa madeni yao.
“Wadeni wameweka akiba ya shilingi bilioni 7, mafanikio makubwa katika wajibu ambao Hustler Fund ilikusudia kutekeleza katika kuhamasisha uwekaji wa akiba za kitaifa,” aliongeza Rais Ruto.
“Najivunia kwamba hatua hizi zimefikiwa hasa kwa mtando wa dijitali na michakato yote imefanywa kuwa ya kidijitali.”
Waziri wa Vyama vya Ushirika Wycliffe Oparanya aliwaongoza maafisa wengine wizara katika kumtaarifu Ruto juu ya utendaji kazi wa hazina hiyo katika Ikulu ya Nairobi leo Jumatano.