Waziri wa Afya Aden Duale amemuomboleza Dkt. Job Obwaka aliyefariki Ijumaa akiwa na umri wa 83.
Kupitia kwa taarifa, Duale alidokeza kuwa Dkt. Obwaka alijitolea kujimarisha katika taaluma ya afya nchini Kenya, huku akiacha mchango wa kupigiwa mfano katika tasnia ya afya kupitia uongozi bora na kukuza vizazi kadhaa kwenye uwanja huo wa utabibu.
Kulingana na ripoti, Dkt. Obwaka ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Nairobi Hospital, alipelekwa hospitalini akiwa amepoteza fahamu na kutangwa amefariki muda mfupi baadaye.
Duale alisema kazi ya Dkt. Obwaka iliimarisha viwango vya ubora vya utunzaji na afya ya uzazi kote nchini.
“Tunaheshimu mchango wake na tunatuma rambi rambi zetu kwa familia na jamii yote ya utabibu wakati huu mgumu,” alisema Duale.