Kenya na Lesotho zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta ya kilimo, ili kufanikisha utoshelevu wa chakula na lishe bora.
Akizungumza aliposhiriki mazungumzo na Waziri wa Kilimo wa Lesotho anayezuru hapa nchini Selibe Mochoboroane, Waziri wa Kilimo wa Kenya Mutahi Kagwe, alidokeza kuwa ushirikiano huo utaboreshwa kupitia ubadilishanaji wa ujuzi, uvumbuzi na ushirikiano wa taasisi.
Aidha, viongozi hao wawili walijadiliana kuhusu kuimarisha ushirikiano wa mifumo ya mbegu, kilimo cha mboga na matunda, ukuaji wa sekta ya mifugo, utafiti na uvumbuzi kwa lengo la kuharakisha mageuzi katika sekta ya kilimo na kuboresha utoshelevu wa chakula katika mataifa hayo mawili.
Wakati huohuo walielezea umuhimu wa kutiwa saini kwa Mkataba wa Maelewano kufanikisha ushirikiano wa kiufundi na ushirikiano wa muda mrefu kati ya taasisi za kilimo kati ya Kenya na Lesotho.