Mtangazaji nguli wa zamani wa Shirika la Utangazaji nchini, KBC Leonard Mambo Mbotela amefariki.
Mbotela alifariki leo Ijumaa, majira ya saa tatu asubuhi, wakati akipokea matibabu katika hospitali moja jijini Nairobi.
Mtangazaji huyo amekuwa akiugua kwa muda.
Mbotela alizaliwa mnamo Mei, 29 mwaka 1960 na hadi kifo chake, alikuwa na umri wa miaka 85.
Alizaliwa katika mji wa Frere huko Mombasa na kusomea katika shule ya msingi ya Frere na kisha akajiunga na shule ya upili ya Kitui.
Baada ya kumaliza masomo, Mbotela katika mahojiano yaliyopita aliiambia KBC kuwa alienda kutafuta ajira mjini Nakuru.
Ingawa alifanya hivyo, ari yake ya utangazaji ilikuwa ikimrindima akilini.
Ni wakati akiwa mjini Nakuru ambapo kipaji chake cha uanabari kilipaliliwa baada ya kujiunga na gazeti la Baraza lililochapishwa mjini humo kama Ripota.
“Ingawa nilikuwa Nakuru, nilitamani ningekuja jijini Nairobi na kujiunga na VoK wakati huo, ” Mbotela alinukuliwa akisema wakati akihojiwa kwenye kipindi cha “Legends Edition” na Catherine Kasavuli, mtangazaji mwingine nguli ambaye pia ametangulia mbele za Mungu.
Tamanio ambalo lilikuja kutimia baadaye alipojiunga na VoK.
Alifahamika sana kutokana na kipindi chake cha “Je, Huu ni Uungwana” kilichopeperushwa kwenye idhaa ya redio na runinga ya KBC.
Kando na kuwa mtangazaji, Mbotela pia alikuwa mwimbaji hodari.