Huduma ya Taifa ya Polisi (NPS) imepuuzilia mbali madai yanayosambazwa katika mitandao ya kijamii yakiashiria kuwa Sadam Buke ambaye ni raia wa kaunti ya Isiolo ametekwa nyara.
Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja, kupitia kwa msemaji wa huduma hiyo Muchiri Nyaga, amesema Buke na wenzake wamekamatwa na wanazuiliwa.
“Tungependa kubainisha kuwa Sadam Buke anazuiliwa na wenzake. Anashukiwa kuwa mwezeshaji mkuu na mratibu wa kundi la Oromo Liberation Front (OLA) katika kaunti za Isiolo na Marsabit,” alisema Kanja kwenye taarifa.
“Alikamatwa wakati wa ‘Operesheni Ondoa Jangili’ inayotekelezwa katika operesheni za Marsabit na Isiolo. Yeye na wenzake wanatarajiwa kuwasilishwa mahakamani.”
OLA ni kundi la wanamgambo kutoka nchi jirani ya Ethiopia na wanachama wa kundi hilo wanashukiwa kujificha humu nchini.