Kundi la nne la polisi wa Kenya limewasili nchini Haiti kwa misheni ya kulinda amani.
Polisi hao ambao wanajiunga na ujumbe wa maafisa wa usalama kutoka nchi tofauti – MSS, waliondoka nchini juzi Jumanne usiku kwa operesheni hiyo.
Kundi hilo la nne la polisi wa Kenya kwenda nchini Haiti, liliwajumuisha wanawake 24 kati ya maafisa 144 wa usalama, na watashirikiana na wenzao walio Haiti kudumisha usalama.
Polisi hao walipokelewa na maafisa wakuu wa serikali ya mpito nchini Haiti, akiwemo Rais Leslie Voltaire na Kamanda wa MSS Godfrey Otunge.
Haiti imekuwa ikikabiliwa na ukosefu wa usalama unaosababishwa na magenge ya wahalifu.
Hata hivyo, hali imesemekana kuimarika ikiwa ni pamoja na katika mji mkuu wa nchi hiyo Port-au-Prince, kutokana na doria zinazofanywa na maafisa wa MSS.
Awali, kulikuwa na hofu kuwa hatua ya Marekani kusitisha ufadhili kwa kikosi cha kimataifa kinachodumisha usalama nchini Haiti itaathiri shughuli za kikosi hicho.
Hata hivyo, katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio, Rais William Ruto amebainisha kuwa operesheni ya kuleta usalama nchini Haiti inayoongozwa na Kenya, itaendelea kupokea ufadhili wa kifedha kutoka kwa serikali ya Marekani.