Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji nchini, KBC, Agnes Kalekye, wakuu wa zamani na wa sasa wa KBC na watangazaji wengine waliofanya kazi na mtangazaji nguli Leonard Mambo Mbotela ni miongoni mwa watu ambao wameomboleza kifo chake.
Kwenye taarifa, Kalekye amemsifia Mbotela akimtaja kuwa mtangazaji nguli wa kweli katika tasnia ya utangazaji.
“Alitabaruku maisha yake kwa kazi ya utangazaji, akiwatia moyo watu wasiohesabika, kwa shauku yake, uadilifu na dhamira yake kwa ubora,” alisema Kalekye.
“Kama mwasisi wa utangazaji, alibadilisha namna tunavyowasiliana na hadhira yetu, na kuacha alama isiyoweza kufutika katika mioyo na fikira zetu kupitia michango ya Je, Huu ni Uungwana kwa jamii.”
Mhariri Mkuu wa KBC Samuel Maina pia aliomboleza kifo cha Mbotela akimtaja kuwa mtu aliyekuwa na ushawishi mkubwa katika tansia ya utangazaji.
“Naenzi siku nyingi ambazo nilitangamana naye ndani na nje ya KBC. Alikuwa mtu mwenye busara na mnyenyekevu,” alisema Maina.
Mtangulizi wake, Vitalis Musebe pia alimwomboleza Mbotela.
“Naomba nitoe rambirambi zangu kwa familia yake. Nilimjua kama mtangazaji hodari na mtu mwenye maadili mema,” alisema Musebe ambaye ni Mhariri Mkuu wa zamani wa KBC.
Mtangazaji wa zamani wa KBC Pauline Sheghu pia aliungana na wanaomwomboleza Mbotela akikumbuka walivyosukuma gurudumu la utangazaji enzi zao.
“Safiri salama Mzee wetu (majee) Leonard Mambo Mbotela. Asante kwa kuwa kielelezo cha haja kwa vizazi vilivyopita, vilivyo na vitakavyokuja,” alisema Sheghu kwenye rambirambi zake.
“Makiwa kwa familia, ulingo wa wanahabari na Kenya kwa jumla.”
Chama cha ODM pia hakijaachwa nyuma katika kumwomboleza Mbotela.
“Tunaunga na nchi nzima katika kuomboleza kifo cha mtangazaji nguli Leonard Mambo Mbotela leo asubuhi baada ya kuugua kwa muda mfupi,” ilisema ODM katika taarifa.
“Leonard Mambo Mbotela alikuwa zaidi tu ya mwanahabari, alikuwa sauti ya hekima, mtambaji, na hazina ya taifa,” alisema Waziri wa Utumishi wa Umma, Justin Muturi.
“Kuanzia enzi za Sauti ya Kenya (VoK) hadi KBC, alitumia mawimbi kutaarifu, kuelimisha na kuhimiza maadili kupitia kipindi maarufu cha “Je, Huu Ni Uungwana?”
Wengine waliomwomboleza Mbotela ni kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna.
Mbotela alifariki leo Ijumaa, majira ya saa tatu asubuhi, wakati akipokea matibabu katika hospitali moja jijini Nairobi.
Mtangazaji huyo amekuwa akiugua kwa muda.
Mbotela alizaliwa mnamo Mei, 29 mwaka 1960 na hadi kifo chake, alikuwa na umri wa miaka 85.