Urban Boys waungana tena baada ya miaka 8

Wataongoza tamasha ya MTN Iwacu Muzika 2026 itakayofanyika huko Rubavu Agosti 1, 2026.

Marion Bosire
2 Min Read

Wanachama wa kundi maarufu la muziki la Rwanda, Urban Boyz, wanaungana tena jukwaani baada ya kutengana kwa miaka minane.

Watatu hao Safi Madiba, Nizzo na Humble Jizzo wataongoza tamasha ya MTN Iwacu Muzika 2026 itakayofanyika huko Rubavu Agosti 1, 2026.

Onyesho hilo litakuwa mara ya kwanza kwa wanakundi hao kutumbuiza pamoja tangu walipotengana mwaka 2019, na hivyo kuhitimisha utengano uliochochewa na uamuzi wa Safi Madiba kuanza safari yake kama mwanamuziki huru.

Safi, ambaye kwa sasa anaishi nchini Canada, aliwasili mjini Kigali Jumanne akiwa ameambatana na Humble Jizzo baada ya wawili hao kusafiri pamoja kutoka Kenya.

Walipokelewa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kigali na Nizzo huku wakianza maandalizi ya tamasha hiyo inayosubiriwa kwa hamu.

Akizungumza mara baada ya kuwasili, Safi alisema anafurahia kurejea nyumbani, huku Humble Jizzo akieleza kuwa kuungana tena kwa kundi hilo ni tukio la kihisia kwa wanakundi na mashabiki wao.

Nizzo naye alisema wana hamu kubwa ya kukutana tena na mashabiki ambao wameendelea kuwaunga mkono kwa miaka yote.

Urban Boyz ilianzishwa mwaka 2008 na baadaye ikawa moja ya makundi yenye mafanikio makubwa katika muziki wa Rwanda, ikishinda tuzo mbalimbali na kutoa nyimbo nyingi zilizotikisa chati za muziki.

Wanamuziki hao pia wameashiria uwezekano wa kushirikiana katika miradi mingine katika miezi ijayo, jambo linalowapa matumaini mashabiki kwamba kurejea kwao kunaweza kuwa mwanzo wa safari mpya ya mafanikio.

Share This Article