Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi ametoa wito kwa Wakenya wakati wote kuthibitisha fursa zote za ajira ughaibuni ili kukwepa mtego wa kulaghaiwa.
Uthibitishaji huo unaweza ukafanywa kupitia njia rasmi za serikali kama vile Wizara ya Kazi, Mamlaka ya Kitaifa ya Ajira, na Idara ya Mambo ya Kigeni.
Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje amewatahadharia Wakenya hasa vijana wanaotafuta ajira ughaibuni dhidi ya kutumia mawakala ambao hawajasajiliwa na kujihadhari dhidi ya ofa za ulaghai.
“Tumesaini makubaliano na nchi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Uingereza, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Qatar, Ujerumani, Austria na hivi karibuni zaidi Italia. Wakati wote tunafuta mipangokazi na nchi zingine,” alisema Mudavadi.
Aliongeza kuwa kupitia mpango wa Kazi Majuu na makubaliano ya kazi ya pande mbili baina ya serikali, Kenya inaunda njia zenye mpangilio, salama na zenye heshima kwa raia wake kufanya kazi ughaibuni.
“Rekodi za hivi karibuni zinaashiria kuwa Wakenya zaidi ya 540,000 wamepata ajira ng’ambo. Fedha zinazotumwa kutoka ng’ambo zilizidi dola bilioni 5 mwaka 2025, na kuzifanya kuwa chanzo chetu kikubwa zaidi cha ubadilishanaji wa fedha. Takwimu hizi zinaelezea siyo tu fursa kubwa iliyopo, bali pia simulizi ya uwajibikaji mkubwa,” alisema Mudavadi.
aliyasema hayo wakati wa warsha na maonyesho ya 4 ya kila mwaka ya uhusiano wa Ajira na Leba (ELRASE IV) iliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Strathmore.

Alidokeza kuwa serikali imefunga mashirika zaidi ya 600 ya kusajili Wakenya wanaotaka kufanya kazi ughaibuni kwa kujiingiza katika mienendo isiyofaa ikiwa ni pamoja na ulaghai.
Aidha, mipango imeanzishwa ya kuwarejesha nchini Wakenya walionaswa katika maeneo ya vita katika mgogoro wa Urusi na Ukraine na pia sakata ya ulaghai wa kimtandao nchini Myanmar.