Makamu wa Rais wa Marekani J.D. Vance amesema kwamba vita vya Marekani na Iran vitaingia katika “hatua tofauti sana” katika miezi ijayo.
Ameyasema hayo katika mahojiano ya kipekee na gazeti la New York Post.
Bw. Vance anaunga mkono kauli za Rais Donald Trump kwamba vita hivyo vitakwisha mara tu baada ya uchaguzi wa katikati ya muhula nchini Marekani.
Katika mazungumzo yaliyofanyika ndani ya ndege siku ya Jumatatu, alisema kuwa Jamhuri ya Kiislamu bado “itapoteza udhibiti wa Lango la Hormuz” kufikia wakati wa uchaguzi.
“Hatuwezi kutabiri wakati ujao, lakini nadhani rais yuko sahihi kwamba hali itakuwa tofauti sana katika miezi michache ijayo,” alisema Bw. Vance.
“Yeye (Donald Trump) pia ndiye Amiri Jeshi Mkuu; kwa hivyo yeye ndiye anayeamua… ni lini migogoro inapoanza na lini inapoisha.”
Makamu wa Rais wa Marekani pia aliongeza: “Ninaelewa vyema kwamba wananchi wa Marekani wanaanza kukosa subira, lakini kinachoendelea kwa sasa ni kwamba Marekani haijajihusisha na operesheni za mashambulizi; kwa kweli hatufanyi hivyo.”
Pia alisema: “Lakini kinachotokea ni kwamba wakati mwingine Wairani hufyatulia risasi meli za kibiashara, ingawa kwa kawaida hawafanikiwi.”
Rais wa Marekani Donald Trump amesema mara kadhaa kwamba vita na Iran vitakwisha baada ya uchaguzi wa katikati ya muhula nchini Marekani mwezi Novemba.
Taarifa ya BBC