Uingereza yaidhalilisha Ufaransa na kutwaa Shaba,Kombe la Dunia

Ilikuwa mara ya kwanza tangu mwaka 1966 kwa Uingereza kushinda nishani ya Kombe la Dunia.

Dismas Otuke
1 Min Read

Bukayo Saka alipachika mabao matatu huku Uingereza, ikiwakalifisha Ufaransa mabao 6-4, na kunyakua nishani ya shaba ya Kombe la Dunia mwaka huu.

Three Lions walianza mechi hiyo ya uwanjani Miami, kwa mekeke huku Nahodha Declan Rice, akiwaweka mbele kunako dakika ya tatu akifyatua tobwe kutoka nje ya kijisanduku na kumwacha hoi kipa Mike Maignon.

Ezri Kosna alitanua uongozi kwa la pili dakika ya 18 ,naye Saka akaongeza mawili dakika za 37 na 46, huku Waingereza wakielekea mapumzikoni kwa uongozi wa 4-0 .

Ufaransa waliamka kutoka usingizi wa pono kipindi cha pili Kylian Mbappe, akikomboa moja dakika ya 48 ,naye
Bradley Barcola akaongeza jingine dakika ya 54.

Mbappe alipiga goli la tatu kunako dakika ya 66,akifikisha mabao 10 katika kipute cha mwaka huu na kuwa mfungaji bora katika historia ya Kombe la Dunia kwa jumla ya magoli 22.

Saka alifanya mambo kuwa 5-3 baada ya kuunganisha mkwaju wa penati dakika ya 87, naye Ousmane Dembele, akapiga goli dakika ya 96.

Nguvu mpya Jude Bellingham, alikongomelea msumari wa mwisho katika jeneza la Ufaransa na kuhitimisha ushindi mkubwa wa 6-4.

Ilikuwa mara ya kwanza tangu mwaka 1966 kwa Uingereza kushinda nishani ya Kombe la Dunia.

Share This Article