Wanafunzi 9 wanaoshukiwa kuteketeza bweni katika shule ya Utumishi Girls Academy wamefikishwa katika mahakama ya Naivasha wakikabiliwa na mashtaka ya mauaji.
Upande wa mashtaka umeomba mahakama kuwazuilia wanafunzi hao kwa siku 30 ili kukamilisha uchunguzi kuhusu mkasa huo wa moto uliosababisha vifo vya wanafunzi 16.
Mahakama itatoa uamuzi juu ya ombi hilo kesho Jumatano.

Wanafunzi 79 walijeruhiwa wakati wa mkasa huo na angalau saba kati yao wanaendelea kupokea matibabu.
Wengine waliruhusiwa kwenda nyumbani baada ya kupokea matibabu.
Maafisa wa upelelezi wanaochunguza mkasa huo, walifanikiwa kuwatambua wanafunzi hao wanaodaiwa kuhusika moja kwa moja katika shambulizi hilo kupitia kamera za CCTV.
Maafisa hao kutoka Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), wamesema wamepiga hatua kubwa kwenye uchunguzi huo.
“Baada ya uchunguzi wa kina kupitia kamera za CCTV kwa usaidizi wa maabara katika idara ya DCI, maafisa waliweza kuwatambua wanafunzi waliowasha moto huo,” ilisema DCI.
Idara hiyo iliongeza kuwa, “Uchunguzi huo ulifanikisha kutambuliwa kwa wanafunzi saba waliohusika moja kwa moja na mkasa huo”.
Shule hiyo kwa sasa imefungwa huku Waziri wa Elimu Julius Ogamba akivunjilia mbali bodi ya usimamizi ya shule hiyo kwa kile alichokitaja kuwa kukosa kuzingatia kanuni za usalama.