Rais William Ruto si sehemu ya tatizo katika mzozo unaoshuhudiwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi ambaye amemshutumu kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka kwa kumhusisha Ruto katika mzozo huo.
“Mzozo unaoshuhudiwa DRC hahusiani kwa vyovyote na Kenya au uongozi wake. Hatupakani na DRC wala hatuna maslahi nchini humo mbali na kuhakikisha amani, uthabiti na ustawi wa watu wake,” amesema Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje kwenye taarifa.
“Kwa hivyo inasikitisha kwamba kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka kwenye picha ya video inayosambazwa katika mitandao ya kijamii anaashiria kuwa Rais William Ruto ni sehemu ya tatizo katika mzozo wa DRC.”
Kulingana na Mudavadi, masuala yanayoikumba DRC yamedumu muda mrefu na ni ya kihistoria na yamejaribu kusuluhishwa na viongozi wa siku zilizopita katika eneo hilo tangu mwaka 1960 hadi sasa.
Ametaja jaribio la Kalonzo kumhusisha Rais Ruto na mzozo nchini DRC kuwa siyo tu kuwa uonevu wa kisiasa bali pia la kizembe kwa kiongozi mwenye hadhi ya Kalonzo ambaye wakati mmoja alihudumu kama Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hii.
Rais Ruto amekuwa mstari wa mbele katika kuwakutanisha viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) katika wadhifa wake kama mwenyekiti wa jumuiya hiyo ili kutafuta mbinu za kusulushisha mzozo nchini DRC.
Viongozi wa jumuiya hiyo pamoja na wale wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wamepangiwa kukutana jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki hii ili kujadiliana juu ya njia mbora za kusuluhisha mzozo nchini DRC.
Hii ni baada ya waasi wa M23 kutwaa udhibiti wa mji wa Goma unaoptikana mashariki mwa DRC katika hatua ambayo imesababisha vifo vya zaidi ya watu 700 na wengine wengi kupoteza makazi.