Watu 710 walikamatwa kote nchini wakati wa maandamano ya kupinga bei mpya za mafuta zilizotangazwa na Mamlaka ya Kudhibiti Petroli na Nishati nchini, EPRA.
Kulingana na Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), waliokamatwa walijihusisha kwenye visa vya uhalifu wakati wa maandamano hayo.
“Visa vya ghasia, uporaji, uteketezaji, ufungaji wa barabara, uharibifu wa mali, mashambulizi dhidi ya maafisa wa polisi na kuhatarisha maisha, ni makosa ya uhalifu,” ilisema DCI.
Idara hiyo ilitoa onyo kwa umma dhidi ya kugeuza maandamano kuwa visa vya uhalifu, ikisema kila Mkenya ana haki ya kushiriki maandamano ya amani na haki ya kujieleza.
Eneo la Rift Valley liliongoza kwa idadi ya waliotiwa nguvuni likiwa na watu 259, kaunti ya Nairobi ilifuata na watu 189, eneo la Kati watu 142, Mashariki mwa Kenya watu 103, Magharibi mwa nchi watu 10 na Pwani watu 7.
“Tayari baadhi ya washukiwa hao wamefikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa makosa mbalimbali,” iliongeza DCI.
Idara hiyo imeonya kuwa wale wanaopanga, kufadhili, kuchochea au kushiriki visa vya uhalifu watakabiliwa kikamilifu kulinagana na sheria.
Wahudumu wa uchukuzi wa umma waligoma siku ya Jumatatu kulalamikia bei ya juu ya mafuta huku wakitatiza shughuli za uchukuzi kote nchini.