KDF yawakumbuka maafisa wake walioangamia kwenye ajali ya helikopta

Tom Mathinji
2 Min Read
KDF yawakumbuka maafisa wake walioangamia.

Maafisa wa Vikosi vya ulinzi hapa nchini KDF, leo Alhamisi waliandaa ibada ya kuwakumbuka wanajeshi walioangamia katika ajali ya helikopta Aprili 18, 2024 katika eneo la Sindar kaunti ya  Elgeyo Marakwet.

Miongoni mwa walioangamia katika ajali hiyo ni pamoja na marehemu Francis Ogolla aliyekuwa Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi wakati huo.

Wengine waliokumbukwa wakati wa ibada hiyo ni pamoja na Brigedia  Swalleh Saidi, Kanali Duncan Keitany, Luteni Kanali David Sawe, Meja George Magondu, Kapteni Mohammed Sora, Kapteni Hillary Litali, Sajenti Mkuu John Mureithi, Sajenti Cliphonce Omondi,na  Sajenti Rose Nyawira.

Maafisa wa KDF walioangamia katika ajali ya helikopta Elgeiyo Marakwet, wakumbukwa.

Wanajeshi hao hawakukumbukwa tu kwa huduma yao kwa taifa, lakini pia kutokana na maadili, ujasiri, kujitolea na uzalendo wa kupigiwa mfano.

Wakati wa ibada hiyo, viongozi wa kidini walihimiza familia zilizoathiriwa kuwa na imani, wakiwahakikishia kuwa licha ya kwamba wapendwa wao wamefariki, wangali hai katika ulimwengu wa kiroho.

Akizungunza kwa niaba ya familia zilizowapoteza wapendwa wao, Charles Magondu, babake marehemu Meja George Magondu, alitambua usaidizi mkubwa walizopokea katika mwaka mmoja uliopita, na kusifu uhusiano dhabiti unaoshuhudiwa katika Vikosi vya Ulinzi nchini.

Wanajeshi wawakumbuka wenzao walioangamia.

Kwa upande wake, kanali Kasaine Ole Kuruta, mmoja wa manusura wa ajali hiyo, alielezea anavyojizatiti katika safari yake ya uponyaji wa mwili na pia kihisia.

Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi hapa nchini  Jenerali Charles Kahariri, alitaja siku hiyo kuwa itakayokumbukwa daima, akitambua huduma muhimu na kujitolea kwa hali ya juu kwa maafisa walioagamia.

Wengine waliohudhuria ibada  hiyo ni pamoja na Naibu Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi Luteni Jenerali John Omenda, Kamanda ya jeshi la Nchi Kavu Luteni Jenerali David Tarus, na kamanda wa jeshi la wanamaji Meja Jenerali Paul Otieno miongoni mwa wengine.

Website |  + posts
Share This Article