Ziara ya Rais William Ruto ya ukaguzi na uzinduzi wa miradi ya maendeleo katika kaunti ya Nairobi, inaingia siku ya pili leo Jumanne, huku akitarajiwa katika maeneo bunge ya Mathare na Ruaraka.
Baadhi ya miradi atakayozindua kwenye ziara hiyo ni pamoja na ujenzi wa bweni la vitanda 800 katika shule ya upili ya St. Teresa Mathare, kuweka jiwe la msingi wa ujenzi wa madarasa 12 katika shule ya msingi ya Mabatini na kukagua ujenzi unaondelea wa madarasa katika shule mseto ya upili ya Mathare.
Kiongozi wa taifa anatarajiwa kuzindua ujenzi wa chuo cha kiufundi cha Mathare ( TVET) na mradi wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu wa Mathare na kisha kukagua ujenzi wa soko la kisasa katika eneo bunge la Ruaraka.

Baadaye, Rais atawahutubia wananchi katika sehemu ya Car Wash kwenye barabara kuu ya Thika, eneo bunge la Roysambu.
Jana Jumatatu, Rais Ruto alizuru eneo la Kamukunji ambako alizindua miradi kadhaa ya maendeleo na pia kutetea ushirikiano wake na kiongozi wa ODM Raila Odinga.
Kulingana na Ruto, ushirikiano huo unalenga kuunganisha Wakenya na kuchangia ukuaji wa kiuchumi wa taifa hili.