Mmoja auawa, kadhaa wajeruhiwa kufuatia mzozo wa ardhi Malindi

Martin Mwanje & Dickson Wekesa
3 Min Read

Mzozo wa ardhi huko Malindi uligeuka kuwa mauti pale mtu mmoja alipopigwa risasi na kuuawa huku mwanamke mmoja mwenye umri wa makamo akiachwa akiuguza majeraha ya risasi. Mwanamke huyo kwa sasa anapokea matibabu katika hospitali ya kaunti ndogo ya Malindi. 

Watu wengine kadhaa walijeruhiwa katika makabiliano makali yaliyotokana na mzozo wa umiliki wa kipande cha ardhi chenye ukubwa wa ekari tatu na nusu kilichopo katika eneo la Kijiwa, kwenye barabara kuu ya Mombasa-Malindi.

Makabiliano hayo yalianza wakati kundi la vijana wenye silaha walipovamia eneo moja la ujenzi na kushambulia wafanyakazi waliokuwa wakijenga ua. Washambuliaji hao waliharibu vifaa na kubomoa sehemu ya ua huo, na kuibua mivutano kati ya makundi hayo mawili hasimu.


Wakati uharibifu ukiendelea, Mwakilishi Wadi wa Shela Twahir Abdulkarim aliongoza kundi la waandamanaji hadi Ofisi ya Naibu Kamishna wa Kaunti Ndogo ya Malindi, akiitaka kuingilia kati dhidi ya ujenzi wa ua huo uliokuwa ukiendelea.

Maandamano yao nayo yalifuatia maagizo ya muda yaliyotolewa na Mahakama ya Ardhi ya Malindi Ijumaa wiki iliyopita, yaliyositisha kwa muda shughuli zozote kwenye kipande hicho cha ardhi kinachozozaniwa. Baadaye, kundi hilo lililelekea kwenye ardhi hiyo kulikozuka makabiliano na kusababisha kufyatuliwa kwa risasi.
Mwanasiasa wa Malindi Jamal Sheikh alimtuhumu mstawishaji wa kibinafsi, Alfred Akunga, kwa kukaidi agizo la mahakama na kutwaa ardhi hiyo kwa nguvu.

 

Diwani wa zamani wa Watamu Ali Didi alisisitiza kuwa ardhi hiyo inamilikiwa na bintiye, matamshi yaliyoungwa mkono na Mwakilishi Wadi wa Shela.  Didi ameapa kupinga kwa udi na uvumba juhudi zozote za kuitwaa ardhi hiyo.

Sheikh alidai juhudi za awali za serikali ya kaunti kusitisha shughuli haramu zilishindikana, na kwamba mstawishaji huyo alidai kuungwa mkono na mwanasiasa mmoja mashuhuri nchini.

Kiongozi wa dini ya Kiislamu Famau Mohamed Famau alilaani kutwaliwa kwa ardhi hiyo, akisema wamemtaka Naibu Kamishna wa Kaunti kuingilia kati na kutatua suala hilo.

Kwa upande wake, Akunga alisimama kidete akisema yeye ndiye mmiliki halali wa ardhi hiyo, akidai aliinunua mnamo mwaka wa 2016 kwa shilingi milioni 10. Aliongeza kuwa ana stakabadhi za kuthibitisha madai yake.

Mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu Victor Kaudo ametoa wito kwa mamlaka za upelelezi kuwachukulia hatua waliomuua mfanyakazi kwenye ardhi hiyo.

Mwili wa marehemu ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya Star mjini Malindi.

Majeruhi wanatibiwa katika hospitali ndogo ya Malindi.

Mamlaka zimeanzisha uchunguzi kuhusiana na suala hilo wakati moshi wa mashaka ukiendelea kufuka katika eneo hilo.

Martin Mwanje & Dickson Wekesa
Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *