Rais William Ruto amepongeza wanariadha wa Kenya ambao walifanya vyema katika mbio za Marathon za jiji la New York nchini Marekani.
Katika kurasa zake za mitandao ya kijamii, Rais alichapisha bango linaloonyesha jinsi wanariadha wa Kenya walinyakua nafasi tatu za mwanzo katika mbio hizo upande wa wanaume na wa wanawake pia.
“Tunasherehekea ushindi wa kihistoria wa wanariadha wetu katika mbio za marathon za jiji la New York ambapo walipata ushindi mkubwa upande wa wanaume na wanawake,” aliandika Rais.
Kulingana na kiongozi wa nchi, ushindi huo unadhihirisha uwezo, nidhamu na moyo wa ufanisi vitu ambavyo ni kielelezo cha taifa letu.
“Pongezi Hellen Obiri kwa ushindi wa rekodi bora mbele ya Sharon Lokedi na Sheila Chepkirui. Ushirikiano wenu na uvumilivu unathibitisha utamaduni wa Kenya wa kukuza mabingwa wa ulimwengu” aliendelea kusema Rais Ruto.
Alitaja pia kikosi cha wanaume kikiongozwa na Benson Kipruto akifuatiwa na Alexander Mutiso na Albert Korir akisema walionyesha talanta halisia ya Kenya.
Naibu Rais Kithure Kindiki naye alifurahikia matokeo ya mbio hizo za New York huku akitangaza habari za ushindi huo kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.
“Ninapongeza watoto wa kiume watatu wa Kenya pamoja na mabinti watatu kwa kufanya nchi yetu ing’ae mbali na nyumbani.” Alinsika Kindiki.
Katika chapisho jingine Kindiki alimpongeza mwanariadha Eliud Kipchoge ambaye anasema anastaafu kutoka riadha kwa njia ya kipekee huku akiacha wanariadha wengine shupavu ambao wataendeleza rekodi nzuri ya Kenya kimataifa.
Hellen Obiri aliongoza kwa upande wa kina dada akimaliza mbio hizo katika muda wa saa 2 dakika 19 na sekunde 51 huku Sharon Lokedi na Sheila Chepkirui wakifuatia katika muda wa saa 2 dakika 20 na sekunde 7 na saa 2 dakika 20 na sekunde 24 mtawalia.
Benson Kipruto na Alexander Mutiso walimaliza mbio hizo katika muda wa saa 2 dakika 8 na sekunde 9 huku Albert Korir akimaliza sekunde 48 baadaye.
