Vifo kutokana na maporomoko ya ardhi Elgeyo Marakwet vyaongezeka

Marion Bosire
1 Min Read

Idadi ya vifo vinavyotokana na maporomoko ya ardhi yaliyotokea katika eneo bunge la Marakwet Mashariki kaunti ya Elgeyo Marakwet imeongezeka hadi 26.

Katika taarifa kwa wanahabari jana, msemaji wa serikali Isaac Mwaura alisema kwamba miili 22 imetolewa kwenye tope kufikia sasa na kusafirishwa hadi Eldoret.

Waziri wa usalama wa taifa Kipchumba Murkomen baadaye aliongeza kusema kwamba miili minne zaidi iliondolewa kwenye eneo la tukio.

Murkomen alisema pia kwamba watu watahamishwa kutoka maeneo ambayo yako katika hatari ya kukumbwa na maporomoko kufuatia mvua kubwa inayonyesha katika eneo hilo.

Harakati za uokoaji zinaendelea zikiongozwa na kundi la maafisa kutoka idara mbali mbali za serikali na mashirika ya usaidizi.

Jeshi limetoa ndege nne aina ya helicopter zinazotumika katika shughuli za utafutaji na uokoaji katika eneo la mkasa, limetuma pia wataalamu wa afya na wale wa kushughulikia majanga.

Mwaura aliongeza kwamba serikali za kaunti zilizo karibu na eneo hilo nazo zimetuma wataalamu wa afya, machine za kuondoa tope kwenye barabara, ambulensi na hata chakula kwa waathiriwa.

Serikali iliahidi kutoa taarifa za mara kwa mara kuhusu mkasa huo na shughuli za uokoaji.

Website |  + posts
Share This Article