Wabunge wasikitikia hali duni ya Magereza nchini

Tom Mathinji
2 Min Read
Kamishna Mkuu wa idara ya Magereza nchini Patrick Aranduh.

Kamishna Mkuu wa idara ya Magereza nchini Patrick Aranduh, alifika mbele ya kamati ya bunge la taifa kuhusu utekelezaji wa katiba, kujibu maswali kuhusu hali ilivyo katika taasisi hizo za kurekebishia tabia.

Aidha kamishna huyo pia alitakiwa kufafanua kuhusu utumizi wa ardhi ya magereza na maslahi ya maafisa wa magereza pamoja na wafungwa.

Wabunge hao walielezea kutorithika kwao na hatua ya kinyonga ya utekelezaji marekebisho, mazingira duni za utendakazi, ardhi ya idara ya Magereza isiyotumika na kashfa za mara kwa mara zinazodaiwa kutekelezwa katika magereza.

Mbunge wa Embakasi ya Kati Mejja Donk Benjamin, alitoa wito wa kufanyiwa ukaguzi wa mahesabu za Magereza, akihoji jinsi fedha zinazokusanywa na idara ya Magereza zinavyotumiwa.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Eric Karemba, alitaka kufahamishwa kuhusu sheria zinazotoa mwongozo kuhusu utendakazi wa wafungwa, akimtaka Kamiashna huyo wa magereza kuelezea ikiwa wafungwa wanadhulumiwa kwa kisingizio cha kuwarekebisha tabia.

Akijibu maswali hayo, Aranduh alishikilia kuwa ardhi ya idara ya Magereza inatumika vyema na kwamba kazi wanazofanya wafungwa sio za kuletea idara hiyo mapato, ila ni za kuwarekebisha wafungwa tabia.

“Ardhi yetu yote inatumika. Wafungwa wanahusishwa kwa kazi za kuwarekebisha tabia, wala sio za kuleta mapato,” alijibu Aranduh.

Aidha Kamishna huyo alidokeza kuwa mswada unaotoa mwongozo kuhusu leba za wafungwa bado unafanyiwa marekebisho.

Mbunge Mary Wamae wa Murang’a, alilalamikia hali duni ya maafisa wa Magereza na wafungwa, akisema wanaishi katika mazingira magumu, akitaka kuelezwa kwanini maafisa hao hawapati marupurupu ya kufanya kazi katika mazingira magumu kama vile walimu.

Akijibu swali hilo, Aranduh alikiri kuna upungufu wa bajeti katika idara ya Magereza, akidokeza kuwa wamesambaza sare mpya kote nchini. Kuhusu marupurupu ya kufanya kazi katika mazingira magumu, Kamishna huyo alisme fedha hizo hutolewa kuambatana na mwongozo wa idara ya Utumishi wa Umma.

Website |  + posts
TAGGED:
Share This Article