Jarvis atishia kumchukulia Peller hatua za kisheria

Marion Bosire
2 Min Read

Jarvis au ukipenda Jadrolita, mwanamitandao maarufu nchini Nigeria ambaye huigiza kama roboti, ametishia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mwanamitandao mwenzake aitwaye Peller.

Jadrolita ambaye jina lake halisi ni Amadou Elizabeth, alitoa onyo hilo kupitia meneja wake kutokana na madai ya Peller kwamba wanamitandao walijipatia pesa kwa njia isiyofaa kupitia mtandao wa TikTok akiwemo Jadrolita.

Peller ambaye jina lake halisi ni Hamzat Habeeb, na ambaye anaaminika kuwa mpenzi wa Jarvis alitoa madai hayo kupitia video aliyochapisha inayomwonyesha akidai kwamba watumiaji kadhaa wa TikTok walishiriki shughuli za utakatishaji wa fedha kupitia zawadi walizopokea kwenye mtandao huo wa kijamii.

Video ya Peller ilisambaa sana mitandaoni na alionekana kuwa na ujasiri kwamba alichokisema ni kweli.

Kampuni ya Aiso Entertainment ambayo inamsimamia Jarvis ilitoa taarifa kwa umma ikisema kwamba imefahamu kuhusu madai ya Peller na kuyapinga.

Ilisema madai hayo sio ya kweli na ni ya kuharibia msanii wao sifa kwa lengo la kupotosha watazamaji wa kazi za Jarvis na kuhujumu uhusiano wa kitaaluma kati yake na kampuni ambazo anashirikiana nazo kikazi.

Peller ametakiwa aombe msamaha katika muda wa saa 48 sawa na siku mbili kupitia taarifa hiyo ya Novemba 2, 2025 la sivyo kampuni ya Aiso Entertainment itatumia njia za kisheria kuondolea Jadrolita lawama na kuwajibisha wahusika wa hujuma dhidi yake.

Website |  + posts
Share This Article