Mwanamuziki anayekua kwa kasi nchini Uganda D Star amezungumzia ushirikiano wa kikazi ambao ulitibuka na msanii wa Kenya Mejja.
Mwimbaji huyo wa wimbo maarufu “Hozambe” alikuwa akizungumza kwenye mahojiano ambapo alielezea jinsi ushirikiano aliotizamia ambao ungetikisa Afrika Mashariki ulitibuka.
Katika video aliyochapisha, D Star anasikika akimlaumu mwanamuziki mwenza ambaye pia ni mwandishi wa nyimbo Mudra D Viral, kwa kile alichokitaja kuwa kutosimamia mawasiliano ipasavyo kwa kutomhusisha.
D Star alielezea kwamba fursa ya kushirikiana na Mejja katika wimbo ilijitokeza alipozuru Kenya kwa mara ya kwanza, wakati ambapo Hozambe ilikuwa inavuma nje ya mipaka ya Uganda.
Anasema Mejja alionyesha nia ya kushirikiana naye katika kufanya remix ya Hozambe na kuanza mara moja maandalizi.
Collabo hiyo Kulingana na D Star ilikaribia kabisa kukamilika kwani Mejja tayari alikuwa amerekodi sehemu zake za wimbo huo na kutuma kwa DJ Horace kwa maandalizi lakini mpango mzima ukabadilika.
Msanii huyo anaamini kwamba mabadiliko yaliyotokea yaliharibu kila kitu kiasi kwamba Mejja alikata tamaa kabisa.
Akiwaza kuhusu fursa iliyopotea, D Star anasema ushirikiano na Mejja ungebadili kabisa maisha yake na kumuinua hadi viwango tofauti.
“Ninakulaumu Mudra kwa kusambaratika kwa mipango ya Collabo,” alisema D Star akiongeza kushangaa mahali angekuwa amefika leo hii kama msanii.