Kesi ya Matonya kusikilizwa mwezi Juni

Kesi hiyo ilitajwa leo katika mahakama ya Shanzu huko Mombasa na itatajwa tena Juni 3, 2026.

Marion Bosire
2 Min Read

Kesi ya ubakaji inayomkabili msanii mkongwe wa Bongo Fleva kutoka Tanzania katika mahakama ya Shanzu, kaunti ya Mombasa nchini Kenya itasikilizwa Juni 17, 2026.

kesi hiyo ilitajwa leo na kuahirishwa hadi Juni 3, 2026 wakati ambapo itatajwa tena, baada ya kukamilishwa kwa baadhi ya stakabadhi muhimu kutoka pande zote mbili.

Matonya alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Aprili 9, 2026, akikabiliwa na shtaka la ubakaji linalodaiwa kutokea Aprili 7, 2026 katika eneo la Josy Joka Apartments, Kaunti ndogo ya Nyali.

Anadaiwa kumuingilia kimwili Mwanamke aliyetambuliwa mahakamani kwa herufi J.G ambaye hakuridhia. Matonya anakabiliwa pia na sktaka jingine kwenye kesi hiyo, la kushika sehemu za siri za mtu mzima bila idhini.

Msanii huyo tayari ameachiliwa kwa dhamana ya Shilingi 500,000 za Kenya sawa na shilingi milioni 10 za Tanzania, akitakiwa kuwa na mdhamini mmoja raia wa Kenya ambaye atawasilisha kiasi sawa cha pesa.

Hati yake ya usafiri ilibakia Mahakamani, huku mamlaka za uhamiaji zikipatiwa taarifa za kumzuia kusafiri bila kibali.

Upande wa mashtaka ilikuwa umeomba kwamba msanii huyo awekewe masharti magumu zaidi ya dhamana, ikiwemo kuzuiwa kusafiri nje ya nchi bila kibali maalum.

Watetezi nao waliomba wapatiwe masharti nafuu na mahakama wakisisitiza kuwa mshtakiwa yuko tayari kushirikiana na Mahakama.

Share This Article