Vyuo vikuu vyamulikwa kisa kuchelewesha nyaraka za ukaguzi

Kamati ya uhasibu wa pesa za umma bungeni imetishia kuwatoza faini wahasibu wanaochelewesha nyaraka hizo.

Marion Bosire
2 Min Read
Tindi Mwale, Mwenyekiti, Kamati ya Bunge ya Uhasibu wa Pesa za Umma

Kamati ya uhasibu wa pesa za umma ya Bunge la Taifa, imelaumu vyuo vikuu kwa kile kinachotajwa kuwa kuchelewa kuwasilisha nyaraka za ukaguzi wa mahesabu ya matumizi ya pesa.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Tindi Mwale ambaye ni mbunge wa Butere, alionya wahasibu wa taasisi hizo kwamba watawajibishwa binafsi kwa kuchelewa au kukosa kuwasilisha stakabadhi za matumizi kwa ajili ya ukaguzi.

Mwale alilalamika kwamba maswali mengi ya Mkaguzi kuhusu matumizi ya fedha katika vyuo vikuu vya umma yanayoelekezwa kwa kamati hiyo, yanatokana na kucheleweshwa huko kwa nyaraka za ukaguzi.

Haya yalijiri katika kikao cha kamati hiyo na Beatrice Inyangala, anayehudumu kama Katibu wa Elimu ya Juu na Utafiti, katika wizara ya elimu.

Kamati ilidurusu ripoti ya afisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa miaka ya kifedha iliyokamilika Juni 30, 2024 na 2025, ikilenga hesabu za Idara ya Serikali.

Mwenyekiti Mwale alionya kwamba huenda wakalazimika kama kamati kutoza faini wale wanaohusika na ucheleweshaji.

Wajumbe wa kamati hiyo, Mary Emaase wa Teso Kusini, Edwin Mugo wa Mathioya na Nabii Nabwera wa Lugari walihoji ni kwa nini wahasibu huchelewa kuwasilisha nyaraka, wakibainisha kuwa ucheleweshaji huo huleta taswira ya ubadhirifu wa fedha za umma.

Inyangala alikiri kuwepo kwa ucheleweshaji huo, akibainisha kuwa vyuo vikuu vingi hushindwa kuwasilisha nyaraka kwa wakati, lakini akahakikishia kamati hiyo kwamba watachukua hatua za kurekebisha hali.

 

Share This Article