Balozi wa Rwanda nchini Kenya Ernest Rwamucyo ameonya kuwa falsafa ya vita vya kimbari bado ni tishio kwa maeneo ya maziwa makuu, akitaja Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, DRC kuwa mfano wa taifa linalokabiliwa na uhasama wa kimbari uliokithiri.
Rwamucyo alisema haya wakati maadhimisho ya 32 ya siku ya ukombozi nchini Rwanda, maarufu kama Kwibohora, iliyofanyika jini Nairobi.
“Mauaji ya kimbari sio tu kumbukumbu chungu ya kihistoria. Inasalia kuwa kweli na hatari kwa vizazi vya sasa. Katika ukanda wetu hususan Mashariki mwa DRC, makundi yenye itikadi kali yanaendelea kueneza uhasama wa kikabila, kujikana nafsi na mawazo ya kuwabagua na kuwaumbua Watutsi wa Congo,” amesema Rwamucyo.
Rwamucyo alihimiza ushirikiano wa kikanda na kutoka kwa jumuiya ya kimatifa ili kumaliza siasa za chuki na itikadi kali kabla hazijanea.

Siku ya Ukombozi ambayo huadhimishwa kila Julai 4, inalandana na Julai 4 mwaka 1994, wakati majeshi ya Rwanda yalisitisha vita vya kimbari dhidi ya Watutsi ambavyo vilisababisha mauaji ya zaidi ya watu milioni moja ndani ya siku 100.
Mkurugenzi Mkuu wa chuo cha Foreign Service Academy Patrick Wamoto, aliyewakilisha serikali ya Kenya katika hafla hiyo, alisema kamwe kumbukumbu za mauaji ya kimbari hazipaswi kusahaulika.
“Mauaji ya kimbari nchini Rwanda yanasalia kuwa historia moja mbaya dhidi ya maisha ya binadamu na kumbukumbu isiyosahaulika ulimwenguni,”alisema Wamoto.