Timu ya taifa ya Kenya ya soka kwa wasichana wasiozidi umri wa miaka 17, imejikatia tiketi kushiriki fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya pili Jumapili jioni, baada ya kuichakaza Afrika Kusini mabao 3-1, katika uwanja wa kitaifa wa Nyayo.
Junior Starlets inayofunzwa na kocha Midred Cheche, ilifuzu kwa Kombe la Dunia kati ya Oktoba na Novemba, mwaka huu nchini Morocco, kwa ushindi wa jumla wa mabao 5-1, baada ya kushinda mkumbo wa kwanza 2-0, wiki jana mjini Pretoria.
Kenya iliyoshiriki Kombe la Dunia kwa mara ya pili tangu mwaka 2024, katika Jamhuri ya Dominica,itarejea kwa fainali za mwaka zitakazoandaliwa Morocco baina ya Oktoba 17 na Novemba 7 mwaka huu.

Starlets watafungua Kombe la Dunia Oktoba 19 kundini E,dhidi ya China,kabla ya kuvaana na Marekani Oktoba 22 na kukamilisha mechi za makundi dhidi ya Samoa tarehe 25 ,Oktoba.