Rais wa Kenya William Ruto amempongeza Rais Samia Suluhu wa Tanzania kwa kuibuka mshindi kwenye uchaguzi wa urais ulioandaliwa Oktoba 29, 2025.
Kupitia taarifa rasmi kutoka kwa afisi ya Rais, kiongozi wa nchi alisema, “Kwa niaba ya serikali na watu wa Kenya na kwa niaba yangu binasfi, ninampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuchaguliwa tena”.
Katika taarifa hiyo, Ruto pia alisema kwamba Kenya na Tanzania zina uhusiano wa kihistoria na malengo sawa kwa ajili ya ufanisi na uthabiti wa raia wake.
Aliomba raia wa Tanzania wazingatie amani na sheria na wadau wa siasa wakumbatie majadiliano na kuvumiliana wanapotafuta suluhu kwa tatizo lililopo sasa ili kulinda demokrasia na uthabiti.
Rais aliahidi kwamba Kenya iko tayari kuendelea kuhusiana kwa njia inayofaa katika harakati za pamoja za kuafikia maono sawa ya eneo la Afrika Mashariki lenye amani, ufanisi na umoja.
Raia nchini Tanzania wamekuwa wakishiriki maandamano kuanzia siku ya upigaji kura Jumatano, Oktoba 29, 2025 wakipinga uhalali wa uchaguzi huo.
Wawaniaji urais wawili wakuu wa upinzani walizuiwa kushiriki uchaguzi huo ndiposa unatiliwa shaka.
Rais Suluhu alitangazwa mshindi wa uchaguzi huo na kukabidhiwa cheti rasmi cha kuchaguliwa Jumamosi iliyopita baada ya kuzoa karibu asilimia 98 ya kura zilizopigwa.
Uapisho wake unatarajiwa kuandaliwa leo Novemba 3 katika uwanja wa jeshi jijini Dodoma, hafla itakayoonyeshwa moja kwa moja kwenye runinga ya TBC.
