Polisi wamkamata mshukiwa wa msururu wa mauaji Thika

Tom Mathinji
2 Min Read
Mshukiwa wa msururu wa mauaji akamatwa Thika, Kaunti ya Kiambu.

Maafisa wa upelelezi wa makosa ya jinai (DCI), wamemkamata Samuel King’ara Kimani ambaye ni mshukiwa wa msururu wa mauaji,anayehusishwa na mauaji ya wanawake wawili  mjini Thika, kaunti ya Kiambu.

Kulingana na DCI kupitia ukurasa wa X, kisa cha kwanza kilinakiliwa March 17, 2025, wakati mwanamke mwenye umri wa miaka 22 Rosemary Njeri Ndekei, alitokewa alipoelekea Thika mjini kununua nguo.

Kutoweka kwake kulisababisha familia yake pamoja na mpenzi wake wa kiume, kuripoti katika kituo cha polisi cha Thika. Mnamo March 18, 2025, wananchi walipata mwili wa mwanamke katika shamba la kahawa katika eneo la Karibaribi.

Kwa kuwa mwili huo haukuwa na stakabadhi zozote za utambulisho, mwili huo ulipelekwa katika makavazi ya hospitali ya General Kago, ili kufanyiwa uchunguzi.

Mnamo March 19, 2025, mwili huo ulitambuliwa na familia yake kuwa wa Rosemary, na baada ya upasuaji, mpasuaji wa maiti wa serikali alibainisha kuwa kifo cha RoseMary kilisababishwa na kunyongwa.

Aidha, kupitia mtandao wa X, DCI iliongeza kuwa kisa cha pili kilinakiliwa March 31, 2025, ambapo mwanamke mwenye umri wa miaka 20 Hellen Wambui Ndung’u, mwanafunzi katika taasisi ya kiufundi ya Gituamba, aliripotiwa kutoweka baada ya kutumwa na mamake kununua chakula katika kituo cha kibiashara cha  Ngorongo, kaunti ya Kiambu.

Sawia na kisa cha Rosemary, mwili wa Wambui ulipatikana siku iliyofuatia katika kichaka, ukiwa umezikwa kiasi kwa udongo.

Mwili huo haukuwa na majeraha, huku majirani wakiutambua kuwa wa mwanamke aliyeripotiwa kutoweka.

Maafisa wa DCI walianzisha uchunguzi wa kina kuhusu mauaji hayo, na kumkamata mshukiwa mkuu Samuel King’ara Kimani, katika eneo la Ngomongo mnamo April 14, 2025.

King’ara anadaiwa kuwapeleka waathiriwa katika shamba la kahawa ambako aliwabaka kabla ya kuwaua.

Alifikishwa mahakamani April 16, 2025, ambapo maafisa wa polisi walikubaliwa kumzuilia huku uchunguzi ukiendelea.

Website |  + posts
Share This Article