Gavana wa Kaunti ya Bomet Hillary Barchok, amekamatwa na maafisa wa Tume ya Maadili na kupambana na Ufisadi (EACC), kwa madai ya kujihusisha na ufisadi.
Barchok alikamatwa, baada ya maafisa wa Tume hiyo kutekeleza operesheni kwenye majengo yanayodaiwa kumilikiwa naye na kwa sasa anazuiliwa katika afisi za EACC kaunti ya Bomet.
Kulingana na EACC, operesheni hiyo ni sehemu ya uchunguzi unaoendelea kuhusu madai ya ukinzani wa maslahi na wizi wa fedha za umma katika kaunti ya Bomet.
Barchok anatarajiwa kufikishwa katika afisi za EACC Nakuru, ili kuandikisha taarifa.
Hatua ya kukamatwa kwa Gavana huyo, inafuatia malalamishi kutoa kwa viongozi wa kaunti hiyo wakimshtumu kwa usimamizi mbaya wa taasisi za umma.
Uchunguzi huo wa maafisa wa EACC ulianza mwezi Oktoba mwaka 2024, uliosababisha kukamatwa kwa maafisa wakuu wa kaunti hiyo.