Kenya na Japani zimeahidi kuimarisha mipango ya ushirikiano wa ulinzi baina yao ikiwemo michango inayotolewa kwa Kituo cha Kimataifa cha Mafunzo ya Ukuzaji wa Amani (IPSTC) na mazoezi ya pamoja kati ya Vikosi vya Ulinzi vya Kenya (KDF) na Vikosi vya Kujihami vya Japani (JSDF).
Ahadi hiyo imetolewa wakati wa mkutano kati ya Waziri wa Ulinzi Soipan Tuya na mgeni wake ambaye ni Balozi wa Japani humu nchini Matsuura Hiroshi aliyemtembelea katika makao makuu ya ulinzi jana Jumatano.
Kenya na Japani zimekuwa na uhusiano thabiti ambao umeimarika miaka nenda miaka rudi kupitia ushirikiano katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na elimu, utunzaji wa mazingira na usalama.
Wakati wa mazungumzo baina yao, Tuya na Hiroshi pia walizungumzia ushirikiano unaoendelea na ujao wa mipango ya usalama kati ya Kenya na Japani ikiwa ni pamoja na fursa za ushirikiano ulioboreshwa kupitia mpango wa Usaidizi wa Usalama wa Japani Nje ya Nchi (OSA) huku kipaumbele kikitolewa kwa usalama wa majini.