Wafanyakazi zaidi ya 200 kupoteza ajira Makueni

Tom Mathinji
1 Min Read
Gavana wa Makueni Mutula Kilonzo Jnr.

Hatua ya Marekani kusitisha huduma za Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID), huenda ikasababisha wafanyakazi 269 kupoteza ajira katika kaunti ya Makueni. Hayo ni kulingana na Gavana wa kaunti hiyo Mutula Kilonzo Jnr.

Kulingana na Gavana huyo, wafanyakazi hao ni wale ambao huwashughulikia wagonjwa wanaougua virusi vya UKIMWI na wale wa Kifua Kikuu.

Kupitia kwa taarifa, Mutula alielezea wasiwasi kuhusu hatima ya miradi ya afya inayofadhiliwa na shirika la USAID, akisema idadi kubwa ya watu hutegemea dawa za kupunguza makali ya virusi vya UKIMWI na Kifua Kiku.

“Licha ya kwamba tumepokea hakikisho kwamba taifa hili lina hifadhi ya dawa hizo zinazoweza dumu kwa muda wa miezi 15, bado kuna changamoto kuhusu swala hilo,” alisema Gavana huyo.

Mutula alidokeza kuwa baadhi ya vituo vya afya katika kaunti hiyo huenda vikafungwa, kutokana na kusimamishwa kazi kwa wahudumu  wa afya ambao walikuwa wakifadhiliwa na USAID.

“Serikali ya Kenya inapaswa kushiriki mazungumzo na Marekani kuhakikisha mpito shwari, ili kuokoa maisha,” aliongeza Gavana huyo.

Rais Donald Trump wa Marekani alisimamisha Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID), kwa madai inafuja pesa na inahitaji kuundwa ili kuendana na vipaumbele vya sera za Rais.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *