Waziri wa Kilimo Mutahi Kagwe amepuuzilia mabali madai kwamba ushuru unaotozwa Majani Chai, unasambaratisha sekta hiyo, akidokeza kuwa ushuru huo ni muhimu kwa utafiti, uuzaji wa zao hilo kwa soko la kimataifa na uongezaji dhamani.
Akizungumza wakati wa kukabidhi kiwanda cha kutayarisha Majani Chai cha Sencha Green Tea kwa wakulima wa Majani Chai wa kampuni ya Kangaita kilichogharimu shilingi milioni 360, Kagwe alisema dhana kwamba ushuru huo unadumaza ukuaji wa sekta hiyo, ni ya kupotosha.
Alidokeza kuwa asilimia 0.08 ya ushuru wa Majani Chai hautozwi wakulima, lakini wanunuzi wa bidhaa hiyo na unapiga jeki uuzaji wa Majani Chai ya Kenya kwenye masoko mapya, unafadhili utafiti, kuimarisha aina mbalimbali za majani Chai na kuimarisha uongezaji dhamani.
“Je, fedha za kupigia debe Majani Chai ya Kenya kwenye soko la kimataifa zitatoka wapi iwapo hatutaunga mkono ushuru huo?.” aliuliza waziri huyo.
Kulingana na Kagwe, mimea ya zamani ya Majani Chai, imeendelea kuchangia mavuno yaliyopungua katika maeneo mengi ya ukuzaji Majani Chai, na kusababisha dharura ya kufanya utafiti wa aina mpya za Majani Chai zilizo na mavuno mengi na zinazostahimili Mabadiliko ya Tabianchi.
Ufufuzi wa kiwanda hicho cha kutayarisha Majani Chai kilichositisha shughuli zake mwaka 2019 kutokana na mzozo wa umiliki, umefadhiliwa na serikali ya Japan, baada ya serikali ya Kenya kuingilia kati.
“Kiwanda hiki sasa kinamilikiwa na wakulima wa Kangaita. Huo ndio ujumbe niliopewa na Rais William Ruto,” alisema Waziri Kagwe.
Kagwe alikariri kujitolea kwa serikali kuwekeza mapato kutoka kwa ushuru wa Majani Chai katika sekta hiyo kupitia utafiti, uvumbuzi na uwezeshaji wakulima, akidokeza kuwa wale watakaofaidika ni wakulima wa Majani Chai kote nchini.