Ruto: Serikali imejitolea kuimarisha uchumi wa baharini

Tom Mathinji
1 Min Read
Rais Ruto azuru chombo cha utafiti cha Dr Fridtjof Nansen, kaunti ya Mombasa.

Rais William Ruto amesema serikali imejitolea kuimarisha uchumi wa baharini kama nguzo ya kimkakati ya kufanikisha utoshelevu wa chakula, kubuni nafasi za ajira na kupanua fursa za kiuchumi miongoni mwa vijana.

Aliyasema hayo Alhamisi katika kaunti ya Mombasa, alipozuru meli ya utafiti kwa jina Dr Fridtjof Nansen inayomilikiwa na Norway na inayohudumu kwa kutumia bendera ya Umoja wa Mataifa na kusimamiwa na taasisi ya utafiti wa baharini.

“Utafiti wa meli hiyo utapanua uwezo wetu wa ufahamu wa rasilimali zilizopo kwenye bahari zetu, kuimarisha ujuzi wetu wa uzalishaji wa baharini na usimamizi bora wa rasilimali,” alisema Rais Ruto.

Kulingana na Rais Ruto, ushirikiano kati ya watafiti  wa chombo hicho na wanasayansi wa Kenya, utaimarisha uwezo wa hapa nchini na kuchangia maendeleo endelevu kwa uchumi wetu wa baharini.

Ziara hiyo ni sehemu ya kongamano la 11 la Bahari Yetu katika kaunti ya Mombasa.

Share This Article