Serikali ya Equatorial Guinea yajiuzulu

Serikali ya Equatorial Guinea imejiuzulu baada ya kushindwa kutimiza malengo yake.

Tom Mathinji
1 Min Read
Manuel Osa Nsue Nsua - Waziri Mkuu wa Equatorial Guinea.

Serikali ya Equatorial Guinea imejiuzulu baada ya kushindwa kutimiza malengo yake. Hayo yametangazwa na Makamu wa Rais Teodoro Nguema Obiang Mangue.

Obiang, ambaye pia ni mwana wa Rais Teodoro Obiang Nguema Mbasogo, alisema Waziri Mkuu aliwasilisha kujiuzulu kwa wanachama wote wa serikali kwa sababu imeafikia tu asilimia 10 ya malengo yake.

Hata hivyo, hakufafanua malengo hayo lakini taarifa kutoka kwa chama tawala ilisema Rais wa taifa hilo alidokeza kuwa serikali imeghubikwa na ufisadi na kushindwa kuimarisha uchumi.

Rais Obiang, ndiye Rais aliyedumu kwa muda mrefu duniani ambaye ameongoza taifa hilo la Magharibi mwa Afrika tangu mwaka 1979, huku akiwateua wanachama wa familia yake serikalini.

Rais huyo aliiteua serikali inayoondoka mwaka 2024 huku Manuel Osa Nsue Nsua akiwa Waziri Mkuu.

Makamu wa Rais wa nchi hiyo alidokeza kuwa kujiuzulu kwa serikali kunaambatana na sera ya uwajibikaji inayohitaji usimamizi wa umma ni sharti ushuhudie matokeo.

Serikali mpya inatarajiwa kubuniwa hivi karibuni.

Share This Article