Takriban watu 20 wameuawa Kaskazini Magharibi mwa Nigeria, baada ya watu waliokuwa na silaha kushambulia vijiji kadhaa katika jimbo la Zamfara.
Kulingana na mwakilishi wa wilaya ya Sauna, uvamizi huo ulitekelezwa kati ya saa tisa na saa kumi alasiri saa za nchi hiyo.
Shambulizi hilo linajiri huku ghasia zikiongezeka Kaskazini Magharibi na eneo la kati nchini Nigeria, ambako makundi ya wapiganaji na majangili wamevamia vijiji wiki kadhaa zilizopita.
Wavamizi hao pia wamedaiwa kuiba mifugo na kuwateka nyara wakazi wa vijiji hivyo.
Siku ya Jumanne, majangili watatu waliuawa na maafisa wa usalama katika jimbo la Kwara, ambapo mfanyabiashara Tuhkur Sanni aliokolewa.
Visa vya utekaji nyara nchini Nigeria vimeongezeka, makundi ya wapiganaji yakiitisha fidia ya kiwango cha juu kutoka kwa serikali na wananchi.
Mwaka 2024, washambuliaji hao walikusanya zaidi ya dola milioni 1.6 kama malipo ya fidia.