Mwanamke afungwa miaka 3 gerezani kwa wizi wa mtoto

Tom Mathinji
1 Min Read
Mwanamke afungwa miaka 3 jela kwa wizi wa mtoto.

Mwanamke mwenye umri wa miaka 26, amehukumiwa kifungo cha miaka 3 gerezani, baada ya kupatikana na hatia ya kumuiba mtoto wa umri wa miaka mitatu, katika kile kinachoaminika kuwa sakata ya mapenzi.

Asha Wanyonyi, aliyewasilishwa mbele ya Hakimu mwandamizi  Jamlick Murithi, alishtakiwa kwa kosa la kumuiba mtoto kinyume na sehemu ya 174(1)(a) ya katiba ya Kenya.

Mahakama hiyo ilifahamishwa kuwa Wanyonyi alimuiba mtoto huyo kwa lengo la kumhadaa Mispher Chepkenoi haki ya kisheria ya kuwa mlezi wa mtoto huyo Machi 20, 2026 katika eneo la Soweto/Kiwerera, kaunti ndogo ya Likoni kaunti ya Mombasa.

Mshtakiwa alikiri mara mbili kosa hilo, licha ya kuonywa na mahakama kuhusu adhabu yake, alishikilia kutenda kosa hilo.

Sakata hiyo ya mapenzi ilimhusisha mshtakiwa, mume wake anyezozana naye, na mpenzi wa mume wake.

Mshtakiwa huyo anadaiwa kuingia kwa nyumba ya mpenzi wa mume wake ambaye alikuwa ameenda kazini na kumuacha mtoto huyo mikononi mwa nyanya yake.

Mshtakiwa alivizia na kuingia nyumbani alimokuwa mtoto huku nyaya yake akiendelea na shughuli za nyumbani, kabla ya kumchukua na kutoroka naye.

Anadaiwa kutoroka na mtoto huyo hadi kaunti ya Bungoma, magharibi mwa Kenya.

Aidha, akiwa safarini ndipo alimfahamisha mama ya mtoto huyo kuhusu hatua ya kumchukua mtoto huyo.

Share This Article