Ruto: Wahamasishaji wa Afya wameimarisha upatikanaji wa huduma za afya

Tom Mathinji
2 Min Read
Rais William Ruto awapongeza wahamasishaji wa afya ya jamii (CHPs).

Rais William Ruto amesema Wahamasishaji wa afya ya Jamii, wamefanikisha upatikanaji wa huduma za msingi za afya katika jamii, akiwataja nguzo kuu katika mfumo wa afya nchini Kenya.

Akizungumza Jumamosi aliposhauriana na wahamasishaji wa huduma za afya kwa jamii katika Ikulu ya Nairobi, Rais Ruto  alidokeza kuwa majukumu yao yanajumuisha uchunguzi msingi wa kiafya ikiwa ni pamoja na shinikizo la damu na sukari, kutambua magonjwa mapema na kuwatuma wagonjwa kwenye vituo vya afya kwa hudumza zaidi za afya.

“Wanawezesha familia kwa kutoa habari za afya hususan kuhusu usafi, lishe bora, afya ya ujauzito, uzuiaji magonjwa na kufanikisha jamii iliyo na afya kuanzia viwango vywa nyumbani,” alisema Rais Ruto.

Kiongozi wa taifa alisema tangu mpango wa wahamasishaji wa afya ya jamii ulipoanzishwa Octoba mwaka 2023 na kuwaajiri wahamasishaji 107,000, wamekuwa nguzo kuu katika kuwaunganisha wananchi na mifumo ya huduma za afya.

Kwenye mkutano huo, Rais Ruto alipigia debe Halmashauri ya Afya ya Jamii (SHA) akiutaja bora kuliko Hazina ya Taifa ya Bima ya Afya (NHIF) iliyotumika awali.

Alisema mpango wa SHA umeimarisha huduma za afya kwa kuongeza ufadhili kwa hospitali za umma, kuongeza usajili wa umma kwa bima ya afya, na kuharakisha utoaji malipo kwa vituo vya afya kote nchini.

Share This Article