Kongamano la Afya 2026 laanza Nairobi

Kongamano hilo la siku mbili linaangazia mafanikio yaliyofikiwa katika sekta ya afya tangu serikali ya Kenya Kwanza ilipoingia madarakani.

Martin Mwanje
2 Min Read

Kongamano la Afya 2026 ambalo ni la kwanza kabisa kuwahi kufanyika nchini limeanza jijini Nairobi. 

Rais William Ruto amewaongoza viongozi wakuu serikalini kuhudhuria kongamano hilo la siku mbili linalofanyika katika Jumba la Mikutano ya Kimataifa la KICC.

Awali, Waziri wa Afya Aden Duale alisema lengo kuu la kongamano hilo ni kuangazia mafanikio yaliyofikiwa na utawala wa Kenya Kwanza katika kuifanyia mabadiliko sekta ya afya nchini.

“Tutanadi mafanikio yetu, na tutatoa takwimu na data. Pili, pia tutaiambia nchi fursa zilizopo kuhakikisha upatikanaji wa afya kwa watu wote nchini na Kenya kuwa namba moja barani Afrika na duniani kote, na kituo bora cha utalii wa afya katika kanda yetu,” alisema Duale.

“Kisha tutaonyesha changamoto ambazo tulikumbana nazo hadi mahali tulipo. Na tutaipa nchi mwelekeo juu ya miaka miwili au mitatu iliyosalia ya Ruwaza ya 2030 na nafasi ya afya katika Ruwaza mpya ya 2060.”

Waziri ameashiria kuwa kongamano hilo linatoa fursa kwa wadau mbalimbali kutoa maoni yao kuhusu mfumo wa afya nchini wakiwemo Wakenya, wahudumu wa afya, vyama vya wahudumu wa afya, wanachama wa Bunge la Mwananchi na viongozi mbalimbali miongoni mwa wengine.

“Afya ni haki. Huu ndio utawala pekee ambao umechukua hatua ya kijasiri ya kutekeleza kipengele cha 43 cha Katiba juu ya afya, elimu, makazi na mengine mengi,” aliongeza Duale.

Tangu uingie madarakani, utawala wa Kenya Kwanza ulianzisha mageuzi mbalimbali katika sekta ya afya kwa kuzindua Mamlaka ya Afya ya Jamii, SHA ili kuchukua nafasi ya iliyokuwa Bima ya Kitaifa ya Afya, NHIF.

Kupitia SHA, serikali inasema Wakenya wengi hasa wa tabaka la chini sasa wamefanikiwa kupata matibabu bila kutozwa malipo katika sehemu mbalimbali nchini.

Kwa mujibu wa takwimu za serikali, hadi kufikia sasa, angalau Wakenya milioni 32 wamejiandikisha na SHA.

Wengine walioajiriwa chini ya mfumo huo ni wahudumu wa afya ya jamii ili kuhakikisha ufanisi wake.

Share This Article