Mapambano dhidi ya kidingapopo yaimarishwa Garissa na Wajir

Martin Mwanje
2 Min Read

Wizara ya Afya imetangaza kuongezwa kwa vita dhidi ya kidingapopo au homa ya dengue ambayo imeripotiwa katika kaunti mbili za Garissa na Wajir.

Katibu Mary Muthoni anasema hadi kufikia juzi Jumatano, kaunti ya Garissa iliripoti jumla ya visa 1,583 huku ile ya Wajir ikiripoti visa 85 vilivyothibitishwa maabarani.

Hii inafanya jumla ya visa vilivyothibitishwa katika kaunti hizo mbili kuwa 1,678.

Huko Garissa, visa 1,276 vya homa hiyo vimeripotiwa katika eneo la Daadab, 251 huko Garissa Mjini huku visa 56 vikiripotiwa katika eneo la Fafi.

Katika kaunti ya Wajir, visa 85 vimeripotiwa kutokea katika eneo la Wajir Mashariki huku visa 10 vikiripotiwa kote katika maeneo ya Eldas, Wajir Magharibi, Wajir Kaskazini, Wajir Kusini, Tarbaj na Khorof Harar.

Wizara ya Afya inasema inafanya kazi kwa ushirikiano na serikali za kaunti na washirika kuchukua hatua mbalimbali za kabiliana na ugonjwa huo.

Hatua hizo zinajumuisha uangalizi ulioboreshwa, kuripoti haraka visa vinavyoshukiwa vya ugonjwa huo huku vituo vya afya katika maeneo yaliyoathiriwa vikitakiwa kuwa macho.

Muthoni amewataka watu kutumia dawa za kufukuza mbu, kuvalia mavazi marefu hasa wakati wa mchana na kuzuia watoto dhidi ya kuumwa na mbu.

Wale walio na dalili za ugonjwa huo kama vile homa, kichwa kuuma sana, kuumwa na macho, maumivu ya misuli na viungo, na kutapika miongoni mwa dalili zingine kutafuta matibabu haraka iwezekanavyo.

Homa ya dengue huambukizwa hasa na mbu aina ya Aedes ambao huuma wakati wa mchana na kuzaliana katika vidimbwi vya maji.

 

Share This Article