Bunge la Tanzania lamuidhinisha Ndejembi kwa kauli moja

Aliungwa mkono na wabunge wote waliokuwepo 324 na hakuna kura iliyoharibika wala ya kumpinga.

Marion Bosire
1 Min Read

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limemuidhinisha Makamu wa Rais Mteule, Deogratius Ndejembi, kwa kauli moja.

Makamu huyo mpya wa Rais alipata kura 324 za wabunge wote waliokuwepo bungeni.

Matokeo hayo yametangazwa leo Agosti 28, 2026 na Katibu wa Bunge ambapo amesema jumla ya kura zilizopigwa zilikuwa 324, na hakuna kura iliyoharibika.

Idadi ya kura za kumpinga ilikuwa sifuri, huku kura halali zikiwa 324. Kwa matokeo hayo, Ndejembi amepata kura zote 324, sawa na asilimia 100 ya kura halali zilizopigwa.

Kutokana na matokeo hayo, Spika wa Bunge ametangaza kuwa uteuzi wa Ndejembi kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umeidhinishwa na Bunge kwa kura 324, sawa na asilimia 100.

Kamati kuu ya halmashauri kuu ya chama tawala nchini humo CCM, ilitangaza uteuzi wa Ndejembi kuchukua nafasi ya Emmanuel John Nchimbi ambaye alijiuzulu.

Katiba ya taifa hilo inaelekeza kwamba wadhifa huo unaposalia wazi, Rais ana muda wa siku 14 kuteua makamu mwingine wa Rais.

Share This Article