Tume Huru ya Uchaguzi na Uratibu Mipaka Nchini, IEBC imetangaza tarehe ya uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Ol Kalou katika Kaunti ya Nyandarua.
Kulingana na IEBC uchaguzi huo utafanyika Alhamisi, Julai 16, 2026, miezi kadhaa baada ya kiti hicho kutangazwa kuwa wazi.
Katika notisi iliyotolewa Jumapili, Aprili 26, tume hiyo ilithibitisha kwamba wapiga kura katika eneo hilo wataelekea kupiga kura kuchagua Mbunge mpya kufuatia kifo cha Mbunge wa eneo hilo, David Njuguna Kiaraho.
Kiti hicho kilitangazwa rasmi kuwa wazi baada ya Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula, kutoa Tangazo kwenye Gazeti Rasmi la Serikali Aprili 20, 2026 akitangaza nafasi hiyo kuwa wazi kwa mujibu wa Ibara ya 101(4)(a) na 103(1)(a) ya Katiba pamoja na Kifungu cha 16(3) cha Sheria ya Uchaguzi.
Aliyekuwa mwakilishi wa eneo hilo bungeni David Kiaraho alifariki Machi 29, 2026, alipokuwa akipokea matibabu katika Hospitali ya Nairobi.
Marehemu mbunge huyo alihudumu kama Mbunge wa Ol Kalou tangu mwaka 2013 na alikuwa katika muhula wake wa tatu mfululizo katika Bunge la Kitaifa.
Tangazo la Wetang’ula lilifungua rasmi njia kwa IEBC kuanza maandalizi ya uchaguzi huo mdogo, unaotarajiwa kuwa ushindani mkali kati ya chama cha UDA kinachoongozwa na Rais William Ruto na chama cha DCP cha aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Jumatano, Aprili 22, 2026 wagombea 10 walijitokeza rasmi mbele ya Naibu Rais Kithure Kindiki, wote wakisaka tiketi ya chama cha UDA kushiriki uchaguzi mdogo wa Ol Kalou.
Wagombea hao walishauriwa kuafikia mwafaka ikiwezekana, huku wakihakikishiwa mchakato wa uteuzi ulio huru na wa haki ndani ya chama, huku kiti cha Ol Kalou kikichukuliwa kama kipimo cha hilo.
Kwa upande mwingine, Gachagua pia alifichua kuwa chama cha DCP kina angalau wagombea tisa wanaowania tiketi ya chama hicho ili kugombea kiti hicho.