Kenya iko mbioni kuimarisha ushirikiano wake na kampuni kubwa duniani ya teknolojia ya matibabu, GE HealthCare, kufuatia mazungumzo ya ngazi ya juu yaliyolenga kuharakisha mageuzi ya sekta ya afya nchini.
Haya ni kulingana na mkuu wa mawaziri ambaye pia ni waziri wa mambo ya nje, Musalia Mudavadi.
Katika taarifa, Mudavadi alisema mazungumzo yake na viongozi wa GE HealthCare yalijikita katika kupanua upatikanaji wa teknolojia za kisasa za matibabu ili kuimarisha mfumo wa afya nchini.
Walijadili pia kuhusu kuendeleza ajenda ya Serikali ya Kufanikisha Huduma Bora za Afya kwa Wote, UHC.
Mkutano huo uliwaleta pamoja Rais na Afisa Mkuu Mtendaji wa GE HealthCare anayesimamia Mashariki ya Kati, Kaskazini Mashariki na Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Uturuki, Urusi na nchi za CIS, Konstantinos Deligiannis, Kaimu Balozi wa Marekani nchini Kenya Susan Burns, Afisa Mkuu Mtendaji wa GE HealthCare Afrika Haroun Mohamed na Meneja Mkuu wa GE HealthCare Afrika Mashariki Alex Oketch.
Kwa mujibu wa Mudavadi, mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha utoaji wa huduma za afya katika matibabu ya saratani, magonjwa ya moyo, pamoja na afya ya mama na mtoto kupitia ubunifu, uhamishaji wa teknolojia na uwekezaji wa kimkakati.
Alisema ushirikiano huo utaimarisha uwezo wa wataalamu wa afya, kukuza mafunzo na ujuzi wa wahudumu wa afya, na kupanua upatikanaji wa huduma bora, nafuu na za wakati kwa wananchi kote nchini.
Mudavadi aliongeza kuwa ushirikiano huo unaonyesha dhamira ya Kenya ya kujenga sekta ya afya ya kisasa na yenye ustahimilivu itakayotoa huduma bora zaidi kwa mamilioni ya wananchi, akisisitiza kuwa ubunifu na ushirikiano imara wa kimataifa ni nguzo muhimu katika kufanikisha mageuzi endelevu ya sekta ya afya nchini.