Wasichana wanane wanafunzi wa shule ya upili ya wasichana ya Utumishi walioshtakiwa kwa mkasa wa moto uliosababisha vifo vya wenzao 16, watasalia kizuizini hadi Septemba 22, 2026.
Wakati huo, mahakama itatoa uamuzi kuhusu ombi la watoto hao la kuachiliwa kwa dhamana.
Uamuzi huu ulitolewa leo na jaji Diana Kavedza wa Mahakama Kuu katika kikao cha kesi hiyo kilichofanyika leo ambapo wanane hao walikanusha mashtaka dhidi yao.
Jaji aliagiza Afisa Msimamizi wa Vifungo vya Nje kuwahoji watu wa familia za wanafunzi walioangamia na walionusurika mkasa huo wa moto shuleni na kuandaa ripoti ya kabla ya dhamana.
Wazazi na walezi wa wanafunzi waliozuiliwa nao walielekezwa walipie huduma za ushauri nasaha za miezi 6 ijayo, ili kuwaelewesha kuhusu sababu ya kutoachiliwa huru kwao kwa wakati huu.
Jaji Kavedza alielekeza pia kwamba wanafunzi hao wasipatiwe simu za rununu na kuwezeshwa kutazama runinga wakati wakatuwa kizuizini.
Kavedza alifungua kikao cha leo na maelekezo yaliyolenga hasa wanahabari ambapo alisema kwamba wasichana hao hawafai kurejelewa kama “washukiwa” kulingana na sheria ya watoto.
Alionya kwamba yeyote atakayerejelea wasichana hao kwa neno hilo ataadhibiwa kisheria.