Msanii wa muziki na mwanabiashara wa Kenya Akothee amelalamikia kile alichokitaja kuwa utambuzi duni wa wasanii katika jamii yake ya Luo.
Lalama zake zinafuatia kifo cha msanii wa muziki wa mtindo wa Ohangla wa lugha ya Dholuo Anthony Ndiema ambaye taarifa za kuaga kwake zilizagaa mitandaoni.
“Karibu kwa jamii ya Luo ambapo unakuwa maarufu baada ya kifo. Wajaluo huomboleza sana kuliko vile wanavyosherehekea na kuunga mkono wasanii wao,” aliandika Akothee kwenye akaunti yake ya Facebook.
Mwimbaji huyo aliendelea kwa kutoa mfano ambapo alikiri kwamba hakuwahi kumfahamu mwanamuziki Abeni jachiga mpaka alipofariki lakini alikuwa anajua wimbo wake kwa jina, “Mano Kasinde”
“Leo ninaona mwanamuziki mwingine wa umri mdogo akiangaziwa kwenye kurasa zote za wajaluo na jumbe za ‘Lala Salama’ na simfahamu,” aliandika Akothee.
Alimaliza kwa kuzomea watu wa jamii yake ya Luo akishangaa ni kwa nini huwa wanaungana tu nyakati za matanga na kusambaratisha wasanii wanaoibuka.
Kulingana na taarifa zilizosambaa mitandaoni, mwanamuziki Ndiema aliaga dunia jana akiendelea kupokea matibabu katika hospitali moja mjini Kisii, baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Anafahamika kwa uimbaji wake wa ubora wa hali ya juu wa nyimbo za Ohangla na Rhumba na alikuwa pia anamiliki bendi ya BBR.