Kenya na Umoja wa Ulaya, EU zimeahidi kuboresha ushirikiano katika nyanja tatu za kimkakati ambazo zitasaidia kuongeza kasi ya Kenya kufikia azima ya kuwa taifa lililostawi zaidi duniani.
Pande hizo mbili zimefikia azimio hilo wakati wa mkutano kati ya Rais William Ruto na Rais wa Tume ya Ulaya, Ursula von der Leyen pembezoni mwa mkutano wa viongozi wakuu wa Kundi la Nchi Saba zilizostawi zaidi kiviwanda duniani, G7 nchini Ufaransa.
Nyanja hizo ni pamoja na kupanua biashara kupitia Makubaliano ya kihistoria ya Ushirikiano wa Kiuchumi yaliyofikiwa miaka miwili iliyopita kati ya pande hizo mbili ya kufungua masoko, kuvutia uwekezaji, na kubuni nafasi za ajira; kuendeleza utoshelezi wa data ili kuifanya Kenya kuwa mshirika wa kuaminika wa kidijitali kwa mtiririko mzuri na salama wa data; na kutumia mpango wa Lango Kuu Duniani kuelekeza uwekezaji katika miundombinu, nishati, na uunganishaji ambao utachochea mabadiliko nchini Kenya.
“Huu ni ushirikiano wenye usawa, unaopimwa siyo kwa msaada, bali kupitia kile tunachojenga, kuwekeza, na kufikia pamoja,” alisema Rais Ruto baada ya mkutano wao.
Kwa upande wake, von der Leyen aliisifia Kenya akisema Ulaya inaichukulia kama kiongozi katika kutatua changamoto zinazoikumba dunia na mshirika wa kutegemewa.
“Biashara yetu tayari imeongezeka kwa kiasi kikubwa. Sasa tunataka kufanya mengi hata zaidi. Kuimarisha uwekezaji na Lango Kuu la Dunia ili kubuni nafasi za ajira na kuunga mkono kupanda kwa Kenya katika mtungo wa thamani. Kuunga mkono uunganishaji bora na mpito safi wa kidijitali,” aliahidi Rais huyo wa Tume ya Ulaya.