Kandarasi hiyo ilitiwa saini na Katibu wa Safari za Ndege na Uendelezaji wa Anga Teresia Mbaika kwa niaba ya serikali ya Kenya, huku kampuni ya CRBC ikiwakilishwa na Meneja Mkuu Yu Xiaodong.
Waziri wa Uchukuzi Davis Chirchir, kupitia ukurasa wake wa X, alisema mchakato wa utoaji zabuni hiyo ulitekelezwa kwa muda wa miezi mitatu, baada ya kukamilika kwa ramani ya JKIA mwezi Februari mwaka huu.
Zaidi ya kampuni 40 zilishiriki kwenye kongamano la kabla ya kutuma maombi ya zabuni lililoandaliwa mwezi Aprili 2026, ambalo lilifafanua matarajio ya mradi huo.
Kulingana na Chirchir, mchakato huo wa zabuni uliandaliwa kwa kuzingatia sheria za ununuzi, huku maombi yote yakikaguliwa kwa kuzingatia uwezo wa kiufundi na kifedha.
Mradi huo unalenga kupanua uwezo wa JKIA, kuimarisha usalama na huduma za kushughulikia mizigo pamoja na abiria, pamoja na kuboresha nafasi ya Kenya kama kitovu cha safari za ndege katika kanda hii.