Kenya imelalamikia vikali hatua ya Israel kuwazuia raia wake kuingia nchini humo kutokana na msambao wa ugonjwa wa Ebola.
Ugonjwa huo umeripotiwa katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Uganda huku angalau watu zaidi ya 150 wakiripotiwa kufariki.
“Kenya inalaani vikali uamuzi wa Israel kuijumuisha Kenya miongoni mwa nchi ambazo wasafiri wake wamezuiwa kuingia nchini humo. Hii hasa inasikitisha ikizingatiwa msaada wa Kenya kwa uangalizi na mwitikio wa kikanda wa ugonjwa wa Ebola,” alisema Katibu wa Wizara ya Mambo ya Nje Korir Sing’Oei kupitia ukurasa wake wa X.
“Huku zaidi ya vipimo 80,000 vikifanywa, hakuna kisa hata kimoja kilichoripotiwa nchini Kenya.”
Kwenye barua yalizoandikiwa mashirika ya ndege Juni 10, Mkuu wa Udhibiti wa Mipaka wa Israel katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Ben Gurion, Amnon Shmueli aliyataka mashirika hayo kutobeba raia wa kigeni na raia wa nchi nne za Afrika Mashariki kuelekea nchini humo.
Nchi hizo zinajumuisha Kenya, DRC, Sudan Kusini, Rwanda na Uganda.
“Zaidi ya hayo, lazima mjiepushe kubeba raia yeyote wa kigeni kwenye ndege kuelekea Israel ambaye amekaa au kutembelea nchi yoyote iliyotajwa hapo juu katika kipindi cha siku 21 kabla ya safari, bila kujali uraia wao au nchi wanamokaa.”
Kenya imeridhia kujenga kituo cha karantini cha kuwatibu raia wa Marekani watakaobainika kuambukizwa ugonjwa wa Ebola nchini DRC.
Ni hatua ambayo imepigwa breki na mahakama na kukumbana na pingamizi kali kutoka kwa wakazi wa Nanyuki ambako kituo hicho kilikusudiwa kujengwa.
Kenya haijaripoti kisa chochote cha ugonjwa wa Ebola hadi kufikia sasa.