Kenya yafurahia makubaliano ya kusitisha vita kati ya Marekani na Iran

Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza kufikiwa kwa makubaliano hayo jana Jumapili kupitia mitandao ya kijamii. Yatasainiwa rasmi Ijumaa wiki hii nchini Uswizi.

Martin Mwanje
2 Min Read
Musalia Mudavadi - Mkuu wa Mawaziri

Kenya imeelezea kufurahia kwake baada ya Marekani na Iran kufikia makubaliano ya kusitisha vita ambavyo vimeathiri uchumi wa dunia kwa kiwango kikubwa. 

Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza kufikiwa kwa makubaliano hayo kupitia mitandao ya kijamii jana Jumapili.

“Serikali ya Kenya inafurahia mno kutangazwa kwa makubaliano ya amani kati ya Marekani na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambayo yanatoa fursa ya kusitishwa kabisa kwa operesheni za kijeshi katika pande zote, ikiwemo Lebanon,” alisema Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi kwenye taarifa leo Jumatatu.

“Tunafahamu taarifa za hafla ya kutiwa rasmi kwa makubaliano hayo Ijumaa, Juni 19 nchini Uswizi, na kupongeza juhudi za kidiplomasia ambazo zimechangia kufikiwa kwa hatua hii,” aliongeza Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje.

Alipendekeza kusuluhishwa kwa changamoto ngumu zinazoikumba dunia kupitia diplomasia jumuishi, kuhesimu sheria ya kimataifa na hekima ya pamoja ya jumuiya ya kimataifa.

Kadhalika, Mudavadi alielezea makubaliano hayo kuwa yanayotoa matumaini ya kusitishwa kwa mzozo kati ya Marekani na Iran, kufunguliwa kwa njia muhimu za usafiri wa majini ikiwa ni pamoja na Mlango Bahari wa Hormuz, na kuleta uthabiti katika eneo pana la Mashariki ya Kati.

Mzozo kati ya Marekani na Iran umedumu kwa takriban miezi mitatu na nusu na kuchangia changamoto nyingi za dunia ikiwa ni pamoja na kupanda kwa bei ya mafuta duniani kote.

Wengi wanatazamia kwamba kufikiwa kwa makubaliano hayo kutasaidia kuleta uthabiti kwa uchumi wa dunia ambao umesusua tangu kuanza kwa mzozo huo Februari 28 mwaka huu.

 

Share This Article