Rais William Ruto mapema leo Jumatatu asubuhi ametia saini kuwa sheria Mswada wa Ugavi wa Mapato 2026.
Hii ni baada ya Bunge la Taifa kuidhinisha mswada huo ambao ulipitia mchakato wa upatanishi baada ya hali ya vuta ni kuvute kuzuka kati ya wabunge na maseneta juu ya kiasi cha fedha kinachopaswa kutengewa serikali za kaunti.
Hafla ya kutia saini mswada huo ilifanyika katika Ikulu ya Nairobi na kuhudhiwa na viongozi mbalimbali, wakiwemo Maspika Moses Wetang’ula na Amason Kingi.
Kufuatia kutiwa saini kwa mswada huo, serikali za kaunti zinatarajiwa kupokea kitita cha shilingi bilioni 428 katika kipindi cha mwaka wa fedha 2026/2027.
Mgao huo wa fedha unatarajiwa kupiga jeki utendaji kazi wa serikali za kaunti wakati ukichochea maendeleo kwa manufaa ya wananchi katika kaunti zote 47 nchini.
Magavana wamekuwa wakilalamikia ukosefu wa fedha waliosema umekwamisha utekelezaji wa miradi muhimu ya maendeleo katika maeneo yao ya utawala.
Kiasi kwamba baadhi ya kaunti zimekuwa hata zikichechemea kulipa mishahara ya wafanyakazi.